Chimbuko/historia ya tahajudi:
Neno tahajudi limetokana na neno la kiingereza linaloitwa ‘meditation’ likiwa na maana ya kufikiri kwa uzingativu au kwa kujali. Neno meditation, nalo limetokana na neno la kilatini linaloitwa ‘meditatio’ likiwa na maana ya mazoezi ya mwili na akili.
Asili ya tahajudi ni dini za mashariki. Ilianzia huko Asia zaidi ya miaka 5,000 iliyopita. Kwa sasa tahajudi hufanywa zaidi huko magharibi (Ulaya na Marekani).
Tahajudi ya miaka hii (ya wakati huu), inazungumzia zaidi tahajudi ya kiyoga ambayo asili yake ni huko India.
Kwa ujumla, tahajudi inaelezwa kama njia za uzingativu katika jambo ambalo mawazo yamelinuia. Lakini pia inaweza kuelezwa kama ifuatavyo:
· Ni hali ya uzingativu na utulivu katika hali halisi ya wakati wa sasa hivi.
· Ni ile hali wakati mawazo yanapokuwa yameyeyushwa na kufikia mahali ambapo hakuna fikra yenye kuingia tena.
· Ni ile hali ambayo, uzingativu, kwa makusudi kabisa umeachwa kuelekea kwenye nguvu kubwa zaidi ( Mungu? Nguvu kuu? ).
· Ni ile hali ya kuweka mawazo na uzingativu katika kitu kimoja, mfano- sanamu ya kidini, pumzi au neno fulani unalotamka (mantra).
· Wengine wanaielezea tahajudi kwamba, ni sala za usiku wa manane.
Tahajudi na dini:
Kila dini ina aina yake ya uzingativu, ingawa ukiutazama kwa undani utagundua kwamba ni tahajudi halisi.
Dini ya kikristo wanatumia rozari, hii huwasaidia kujenga uzingativu. Waislamu wanatumia tasbihi ambayo huwasaidia kujenga uzingativu, lakini pia huwa wanakuwa na sala za usiku wa manane (tahajudi). Wabudha huwa wanafanya tahajudi kila siku kwani ndiyo nguzo yao kuu. Wabahai, hufanya tahajudi kila baada ya sala.
Faida za tahajudi:
Ili uweze kutambua faida za tahajudi, ni muhimu kuifanya kila siku, ikiwezekana asubuhi na jioni. Tahajudi ina faida nyingi sana, faida hizi utaziona tu kama utafanya tahajudi kila siku. Hivyo, tahajudi inahitaji nguvu kubwa sana ya kujituma (wheel power). Ina faida kubwa sana, hivyo ni vizuri ukajenga mazoea ya kuifanya kila siku. Nakushauri, kama huwezi kufanya tahajudi, basi ni afadhali ujifunze upendo ingawa, ni rahisi mara kumi kufanya tahajudi kuliko kuwa na upendo. baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo:
1. Husaidia kuongeza ubora wetu kiakili, kimwili pamoja na uwezo wetu kwa ujumla. Husaidia kuuburudisha mwili, pia husaidia kupumzisha akili na mwili.
2. Husaidia kujenga uzingativu na kukuwezesha kumudu kupata suluhu ya matatizo kirahisi.
3. Husaidia kuratibu msukumo wa damu pamoja na usafirishwaji wa damu mwilini.
4. Husaidia pumzi pamoja na kurahisisha usagwaji wa chakula mwilini.
5. Husaidia kuimarisha mfumo wa kinga mwilini.
6. Husaidia kuleta furaha ya nafsi.
7. Husaidia kuimarisha nguvu yako ya machale pamoja na nguvu zako za ziada.
8. Husaidia kutibu matatizo mengi ya kisaikolojia kwani hubadili hali ya mfumo wa fahamu na mawazo (endapo itafanywa kila siku).
9. tahajudi pia inaweza kutumika kuomba kitu unachohitaji, kama vile kazi au mahitaji mbalimbali, ingawa inashauriwa uwe mwangalifu badala ya kufanya kazi unaweza ukawa mtegemezi wa tahajudi. Mfano, unaweza ukatumia tahajudi kuomba shilingi laki moja na ukapata bila kufanya kazi yoyote au kwa kufanya kazi kidogo sana ambayo hailingani na malipo ya laki moja.
Je, tahajudi huleta utajiri?
Ni swali gumu kwa sababu, utajiri ni dhana pana sana, inategemea tu unazungumzia utajiri upi, wa kitu gani na wapi. Hata ule utajiri wa kimazoea, nao bado ni mgumu kuuelezea. Mfano, tajiri wa kijijini, akihamia mjini anaonekana ni mtu wa kawaida kabisa kwani kuna matajiri wengi sana wanaomzidi.
Lakini, swali la kujiuliza ni hili, unataka utajiri ili iweje au upate nini? Kama unataka utajiri ili uwe maarufu kwa kuandikwa na magazeti, ukweli ni kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuandikwa na magazeti ingawa siyo kwa utajiri ila kwa kubaka mtoto. Lakini pia kama unataka utajiri ili ukupe furaha na amani, ukweli utabaki palepale kwamba, hata kama utaupata huo utajiri, furaha au amani haitapatikana kwani utakuwa umevunja kanuni ya maisha kwani hukuja duniani kutafuta utajiri, bali kuishi kwa kufanya kazi unayoipenda sana, inayokupa furaha na amani bila kujali maslahi, heshima au umaarufu kutoka kwenye kazi hiyo. Kwa kuwa, kazi hii unaipenda, utaifanya kwa ufanisi mkubwa sana, na ndipo utajiri utakapokuja. Kanuni ya maisha kuhusu utajiri inaanza na kufanya kazi inayokupa furaha na amani na ndipo utajiri unafuata, haianzi na utajiri na ndipo furaha na amani vipatikane. Kama huamini, wachunguze matajiri unaowafahamu, ambao walipata utajiri ili uwape furaha na amani, utagundua kwamba, hawana furaha wala amani. Kwa upande wa pili wa shilingi, wale matajiri ambao, utajiri wao ulikuja kupitia kwa kufanya kazi inayowapa furaha na amani, utagundua kwamba wana furaha na amani kubwa sana.
Swali lililoulizwa hapo juu linasema, je, tahajudi huleta utajiri? Kama utajiri ni kupata furaha na amani ya nafsi, jibu ni ndiyo. Hii ni kwa sababu, tahajudi hukusaidia au kukufundisha namna bora kabisa ya kupumzisha akili na mwili na hivyo kuwa mtu mwenye furaha na amani. Kumbuka, ukishakuwa mwenye furaha na amani, wewe tayari ni tajiri wa mali pia.
Tahajudi ina madhara yoyote?
Kwa watu wenye matatizo ya kifafa, matatizo makubwa ya moyo au wenye matatizo ya akili, tahajudi inaweza kuwaumiza wasipokuwa waangalifu, ingawa kwa upande mwingine, tahajudi ni tiba/dawa kwao. Hivyo, wanashauriwa wachague tahajudi ambayo haitawaletea matatizo.
Ni vizuri wakajaribu aina tofauti tofauti ya tahajudi, halafu wakaangalia ni ipi inawasumbua na ni ipi inawapa nafuu. Wakishapata inayowapa nafuu, ni vizuri wakaendelea kuifanya mara kwa mara. Baada ya muda, watagundua kwamba, matatizo yao ya akili, moyo au kifafa yamepungua kwa kiwango kikubwa sana au yameisha kabisa.
Jinsi ya kufanya tahajudi:
Mbinu za kufanya tahajudi hutofautiana kutokana na kiwango cha uzingativu, uwezo wa kujenga taswira na namna mtu anavyoweza kukabili mawazo yanayomwingilia wakati anafanya tahajudi yake.
Baadhi ya mbinu hizi, humfanya mtu apotelee kwenye kile anachozingatia na kutoingiliwa kabisa na wazo lolote. Mbinu hizi ni rahisi mtu kujifunza mwenyewe, ingawa kuna baadhi zinahitaji awepo mwongozaji.
Hatua zinazotakiwa wakati unajiandaa kufanya tahajudi ni kama ifuatavyo:
1. Tafuta sehemu iliyotulia, isiyo na makelele. Kaa kwenye kiti au chini, au lala kitandani. Hakikisha huumii mahali popote. Legeza mwili wako pamoja na misuli yote ya mwili wako kwa kadri utakavyoweza.
2. Sahau matatizo yako yaliyopita, yaliyopo na yajayo. Sahau matatizo yako ya kazini au nyumbani. Jitahidi usifikirie chochote. kama kuna mawazo yataingia, usigombane nayo, usiyape muda na nafasi, wewe endelea na kile ulichoamua kukizingatia. Hakikisha uzingativu wako ni mkubwa. Pia kione hicho unachokizingatia kwa jicho lako la ndani, kijengee taswira kana kwamba unacho tayari au kana kwamba unakiona (unacho).
3. Ni muhimu sana kujali hisia zako wakati unafanya tahajudi. Kwa mfano, kama unafanya tahajudi ya kujenga nyumba. Hakikisha hiyo nyumba unaiona ilivyo, ingia ndani ya hiyo nyumba, sebuleni, chumbani, chooni, stoo, jikoni na sehemu ya kulia chakula (dining). Kila unapoingia, onyesha hisia zako, jione una furaha ndani mwako na ikiwezekana tabasamu, pia jione una amani ndani mwako. Ukweli ni kwamba, utakapokuja kujenga hiyo nyumba, zile hisia ulizokuwa unazionyesha wakati unafanya tahajudi, zitajitokeza au utaziona. Kama tahajudi yako ulikuwa unaifanya ukiwa na huzuni, hali hiyo itajitokeza baada ya kumaliza kujenga nyumba yako. Inaweza ikatokea baada tu ya kujenga nyumba yako, ndugu zako au wa mkeo wakajaa pale nyumbani, wakawa wanafanya vurugu ambazo zitakuletea huzuni na hivyo kuanza kujuta ni kwa nini umejenga hiyo nyumba.
Ukweli ni kwamba, tatizo siyo ndugu, tatizo ni wewe mwenyewe, ni hisia zako ulizokuwa unazionyesha wakati unafanya tahajudi yako ya kujenga nyumba. Na kama wakati unafanya tahajudi yako ulikuwa na hisia za furaha, hali hiyo pia itajitokeza baada ya kumaliza nyumba yako. Hata kama ndugu wa mkeo au mumeo watajaa pale nyumbani, vicheko, tabasamu na mambo mengine ambayo yatakupa furaha yatatamalaki pale nyumbani. Kwa hiyo, hisia ni muhimu sana wakati unafanya tahajudi.
4. Pumua kwa kuingiza pumzi ya kutosha mapafuni, halafu toa pumzi yote na kufanya kifua kiwe kama kitupu. Weka mawazo yako yote kwenye pumzi zako. Vuta pumzi kwa kina kiasi ili oksijeni iingie nyingi zaidi. Unapotoa pumzi unafanya msuli wa mapafu kujisafisha bila kukwazwa. Ni muhimu kuvuta na kutoa pumzi kwa kina angalau mara tatu kabla ya kuanza kufanya tahajudi yoyote.
5. Kila siku asubuhi baada tu ya kuamka na jioni au usiku baada ya watu wote kulala (au usiku wa manane), tenga dakika kumi na tano au zaidi kwa ajili ya kufanya tahajudi. Kuna wakati utakuta mwili hautaki, lakini jenga utashi mkubwa zaidi ya mwili hadi uzoee. Ukiahidiwa safari ya bure ya kwenda ulaya kutembea na ukaambiwa ndege itaondoka saa kumi usiku, nina uhakika ikifika saa saba utakuwa macho au yamkini unaweza usilale kabisa. Lakini pia ikitokea ukaahidiwa kutiwa au kumtia kila siku saa nane mchana na umpendaye sana, nina uhakika utafika kwenye eneo saa sita au saa saba mchana, hata chakula hutakumbuka. Ninakuomba ujenge utashi wa aina hii kwenye tahajudi.
6. Ukipata muda, kama huna kazi ya kufanya, ukiwa peke yako, ofisini, nyumbani, kwenye basi/daladala, kituoni, jaribu kufanya tahajudi. Mazoezi ya tahajudi hufanyika mahali popote.
7. kama ukifanya vizuri tahajudi, utahisi nafuu fulani kimwili au kiakili ama vyote. Utagundua kwamba, mwili hasa upande wa msukumo wa damu, utakuwa na mabadiliko.
Aina za tahajudi:
1. Tahajudi ya pumzi.
Ni kongwe zaidi. Ilianzia china na India. Ni tahajudi nzuri au muhimu kwa wale wanaoanza kujifunza.
Jinsi ya kuifanya: tafuta sehemu tulivu, kaa chini,kwenye kiti au lala kitandani (chali). Hakikisha mwili wako hauumii mahali popote, legeza misuli na viungo vyako vyote vya mwili, fumba macho yako. Vuta pumzi kwa kina halafu iruhusu itoke taratibu, wakati pumzi inatoka unaweza kutaja neno ‘moja’ au ‘one’ au neno lolote ambalo ni rahisi kwako. Usitaje neno hilo kwa mdomo, litaje kwa kulifikiri (kimoyomoyo) na baada ya muda utalizoea, litakuwa linakuja lenyewe.
Faida yake: husaidia kupumzisha mwili na akili.
2. Tahajudi ya mkono:
Hii inakuonyesha ni kwa jinsi gani mawazo yako yana nguvu zaidi kuliko mwili. Lakini pia inakuonyesha uhusiano uliopo kati ya mawazo yako na mwili wako.
Jinsi ya kuifanya: kaa kwenye kiti kisichokuwa na mkono. Miguu ikanyage chini na uweke mikono yako magotini (juu ya mapaja). Fumba macho, tulia, usiwaze kitu chochote, mawazo yakija usishindane nayo, usiyape nafasi wala muda, wewe endelea kutulia.
Ukiwa katika hali ya kupumzika na kufumba macho, chagua kati ya mkono wako wa kulia au kushoto na kupeleka mawazo (ufahamu) wako hapo. Peleka ufahamu wako kwenye mkono uliouchagua (mfano wa kulia). Fahamu kuwa sasa unaufahamu mkono wako wa kulia, yaani unauona kwa macho ya mawazo yako (kumbuka mawazo yetu yana macho, yanaweza kuona kitu hata kama hakipo mbele yetu).
Kwa kutumia macho ya mawazo yako, kitazame kiganja chako cha mkono wa kulia, kifahamu kabisa jinsi kilivyo huku ukiwa umefumba macho. Halafu kwa macho ya mawazo yako, itazame damu inavyozunguka kwenye mkono na kiganja chako, endelea kukitazama kiganja cha mkono huo wa kulia, kitazame kwa mbele na nyuma (ndani na nje). Halafu itazame damu inayotiririka ndani ya kiganja hicho. Wakati unaendelea kukitazama kiganja chako kwa macho ya mawazo yako, kuna mawazo yanapita kwenye ufahamu wako na kukuondoa kwenye uzingatifu wako. Usijaribu kushindana na mawazo hayo, yaache, bali endelea kuweka nguvu yako kwenye kiganja na damu inayotiririka ndani ya kiganja. Endelea kukitazama kiganja chako tena na tena na tena. Sasa hama kwenye kiganja na kitazame kidole gumba cha mkono wako, endelea kukitazama na baada ya muda, hamisha ufahamu wako na kukiona kidole cha pili, cha tatu, cha nne na cha tano yaani cha mwisho. Baada ya hapo, hamisha mawazo yako na kutazama katikati ya paji lako la uso, ni wazi unafahamu vizuri jinsi paji lako la uso lilivyo, endelea kulitazama kwa muda. Jaribu kukadiria umbali uliopo kati ya paji lako la uso na kiganja chako.
Baada ya hapo, endelea kukitazama kiganja chako kwa ndani, ione damu inayotiririka kwenye kiganja chako, tumia muda kidogo kuiangalia. Halafu angalia kiganja chako kwa juu(nje), kione vizuri jinsi kilivyo, peleka ufahamu wako kwenye kidole gumba, kidole kinachofuata, yaani cha pili, cha tatu, cha nne na cha tano. Peleka ufahamu wako kwenye paji lako la uso, endelea na zoezi hili kama ilivyoelezwa hapo juu. Baada ya muda, kama umejenga uzingativu wa kutosha kwa kufuata maelekezo, utaona mkono wako umeanza kupanda wenyewe. Na kama utaendelea kufanya zoezi hili, mkono wako utapanda na kugusa paji lako la uso. Na kama utaendelea kufanya, mkono utashuka wenyewe baada ya kugusa paji lako la uso na kutelemka chini mpaka kwenye paja lako na ukiendelea utapanda tena na kushuka tena.
Faida yake: husaidia kupumzisha mwili na akili, husaidia kutuliza maumivu ya mwili, husaidia kujenga uzingativu, n.k.
3. Tahajudi ya mshumaa.
Jinsi ya kuifanya: Tayarisha mshumaa na kiberiti. Kaa chini au kwenye stuli. Weka mshumaa wako mbele yako kwenye stuli au kitu chochote ili mradi uwe usawa wa macho yako. Uwashe na uanze kuuangalia kwa kuukazia macho bila kupepesa kope. Ukishindwa, pepesa kidogo halafu endelea kuuangalia bila kupepesa tena. Endelea kuuangalia kwa muda usiopungua dakika 10 au 30. Pia, unaweza kutumia moto huu wa mshumaa kuchoma mambo ambayo uliambiwa huwezi. Mfano, uliambiwa huna akili, hivyo, chukua hili neno na lichome kwenye moto huu wa mshumaa. Kama utakuwa umezingatia sana, utaona moto wa mshumaa ukiongezeka au ukibadilika rangi.
Tahadhari: wakati unachoma, usije ukachoma yale mambo mazuri uliyoambiwa.
4. Tahajudi ya mtoto wa ndani:
Hii ni kwa ajili ya kufuta mambo ambayo uliambiwa huwezi. Huwa tunasema, ongea na mtoto wako wa ndani. Jinsi ya kufanya: kaa chini, kwenye kiti au lala kitandani (chali). Jenga taswira ya picha yako ulipokuwa mtoto. Jione mahali ulipokuwa kama ni nyumbani au shuleni. Angalia yale maeneo ambayo unayakumbuka na ambayo uliambiwa huwezi. Kila unapofanya chagua eneo moja moja ambalo unakumbuka uliambiwa hufai. Baada ya kutengeneza taswira ya mtoto huyo ambaye ni wewe, rudi kwako sasa ukiwa mtu mzima. Anza kuongea na huyo mtoto ambaye ni wewe pia. Mwambie kwamba, uliambiwa huna akili (kama uliambiwa huna akili) na wewe ukaamini kwa sababu ya utoto, lakini sasa umekua, fahamu ukweli huu kwamba wewe una akili sana sawa na mtu yoyote. Endelea kurudiarudia hayo maneno kwa muda wa dakika tano au zaidi.
Unapoongea na mtoto wako wa ndani mara kwa mara, pamoja na kukupa faida zingine za tahajudi, itakusaidia pia kukuwezesha kujiamini katika hayo maeneo ambayo uliambiwa huwezi au hufai.
5. Tahajudi ya namba:
Hapa, unatakiwa kuhesabu namba kinyumenyume huku ukiwa umefumba macho. Unaweza ukaanzia 100, 99, 98, 97, 96, …mpaka 1, au unaweza kuanzia 200, 198, 196, 194, 192, … mpaka 2. hakikisha wakati unahesabu namba hizi hukosei, na ikitokea ukakosea namba yoyote hata kama umekaribia kumaliza, itakulazimu kuanza upya. Tahajudi hii ni nzuri sana kwa kurejesha kumbukumbu, ingawa pia ina faida nyingine.
6. Tahajudi ya maua:
Tafuta ua la rangi nyekundu, kijani, njano au nyeupe. Hapa usifumbe macho. Liweke mbele yako na uliangalie kwa kulikazia macho bila kupepesa kope. Hakikisha mawazo, fikra na uzingativu wako wote unaupeleka kwenye ua hilo. Lakini kama una bustani ya maua, unaweza kwenda kukaa bustanini na kuanza kuyaangalia maua hayo kwa kuyakazia macho huku mawazo na uzingativu wako wote ukiwa kwenye ua ulilolichagua.
7. Tahajudi ya rangi:
Hii hutumika kwa ajili ya kujiponya kwani kila rangi inatibu magonjwa fulani kwenye mwili wako kama utaiangalia kwa muda mrefu au kama utavaa nguo ya rangi hiyo. Unaweza ukatumia tunda lenye rangi husika, mfano matunda damu au nyanya kuwakilisha rangi nyekundu.
8. Tahajudi ya sauti:
Hii inahusisha kutaja neno kimoyomoyo ambalo ukishalizoea neno hili itafika mahali huhitaji kulitaja ila utalisikia neno hilo likijitaja lenyewe. Unaruhusiwa kuchagua neno lolote ambalo ndiyo litakuwa nguzo yako ya kujenga uzingativu. Mfano, amani, mungu, furaha n.k.
9. Tahajudi ya kusogea:
Hii huhusisha kuikabili ardhi kama kitovu cha nguvu, huhusisha kusogea kwa aina fulani. Watu wengi hupenda kuifanya usiku.
10. Tahajudi ya kujikagua:
Huhusisha kujikagua baadhi ya maeneo yako ya mwili kwa kutumia macho yako ya akili.
11. Tahajudi ya ukuaji:
Ni tahajudi ambayo imefanyiwa utafiti mwingi sana wa kisayansi na kuthibitishwa kwamba, tahajudi husaidia mwili, akili na hisia, pia ni rahisi kujifunza. Katika tahajudi hii, kila mmoja hupewa neno ambalo hatakiwi kumpa mtu mwingine. Neno unalifanyia kazi ili kujenga uzingativu.
Hizi ni baadhi tu ya tahajudi ambazo huwa zinatumika mara kwa mara. Unachotakiwa ni kuwa mbunifu ili na wewe ubuni tahajudi ya kwako (za kwako) na kuzipa majina yoyote unayotaka. Kwenye maisha hasahasa katika tahajudi, hutakiwi kuwa kasuku wa kutumia tahajudi zilizobuniwa na watu wengine, fanya kila uwezalo kubuni tahajudi yako hata kama ni ndogo kiasi gani ili mradi inakusaidia kukupa uzingativu. Kumbuka kwamba, tahajudi inaweza kufanywa muda wowote na mahali popote.
Usikubali mwili ukutawale kwa kukuambia umechoka na hivyo nenda kalale. Hivi, kuna kitu kinaitwa kuchoka ambako kutakufanya ushindwe kufanya tahajudi? Kama jibu ni ndiyo, jiulize swali hili: umetoka kazini, umechoka sana na unataka kwenda kulala hata kuoga huwezi, halafu kabla hujanyanyuka kwenda kulala, ukamuona nyoka anaingia ndani je, utaendelea kulala au utanyanyuka ili umpige nyoka huyo? Bila shaka, usingizi na uchovu wote utaisha. Unaonaje kama tahajudi itachukua nafasi ya nyoka? Inawezekana! Maelezo haya yanakuonyesha kwamba, hakuna kitu kinachoitwa kuchoka ila wewe unasemaje!
3 hours of Meditation Music
Youtube Video
Kwa leo naishi hapa, kama kuna mwenye changamoto, namkaribisha ili tupate kuelimishana.....
No comments:
Post a Comment