WORK EVENTS WORKS

WORK EVENTS WORKS
CHECK WITH US ALL ABOUT

Wednesday, June 17, 2015

MBINU ZA JINSI YA KUFIKIA MALENGO.

Kwa wengi wetu, mwaka mpya huja na malengo mapya. Ingawa kimsingi tarehe 31 December huwa haitofautiani sana na tarehe 1 January kimtazamo, kwa wengi ni siku tofauti na nafasi ya kipekee ya kujikagua na kujiwekea malengo mapya. Nilipotizama vizuri kalenda ya mwaka 2014 niligundua kwamba tayari mwezi wa kwanza[Januari] umeshakatika. Pengine,kama wewe, kihoro cha kutimiza au kutotimiza malengo kimeshaanza kukunyatia. Waswahili tuna msemo wetu; “siku njema huonekana asubuhi”. Ni kweli. Lakini binadamu tumepewa uwezo wa kubadili mwelekeo wa siku. Tukidhamiria.

Mojawapo ya malengo ambayo wengi wetu tumekuwa tukijiwekea mara tu kengele za kuashiria mwaka mpya umeingia zinapolia, ni pamoja na kujitahidi kuwa na afya nzuri zaidi. Mtu ni afya. Dhamira zetu huwa ni kula vizuri zaidi [na siku hizi na hivi Vyakula vyetu vya makopo hali ni tata zaidi], kushiriki katika mazoezi, kupumzika nk. Tunayo pia malengo mengine mengi. Kuwa mtu mwema zaidi, kuweka akiba zaidi benki, kusoma na kufaulu zaidi, kutembelea ndugu na jamaa zaidi, kupata ajira nzuri zaidi, kuanzisha biashara binafsi. Malengo lukuki.

Pamoja na kujiwekea malengo na kuwa na shauku kubwa ya kutimiza malengo hayo,ukweli ni kwamba wengi wetu huishia katikati ya safari au hata robo tu. Tunashindwa.

Katika makala hii nitagusia mbinu 10 ambazo zinaweza kukusaidia katika kutimiza malengo tunayokuwa tumejiwekea wakati ule tunapokumbatiana, kupeana mikono ya kutakiana kila la kheri kwa mwaka mpya.


  • Weka Malengo Halisia Na Yanayotimizika: Lazima tukubali ukweli kwamba yapo baadhi ya malengo ambayo huwa tunajiwekea mwaka unapoanza ambayo ni kama ndoto za Alinacha. Kwa mfano,unapoweka malengo ya kununua nyumba ya milioni 500 ndani ya mwaka huu wakati akiba yako inasoma kwamba una Shilingi Laki 2, kimsingi uwezekano wa kutimiza lengo hilo ni mdogo labda tu kama utakuwa unapanga kuiba au La Haula ushinde bahati nasibu [kitu ambacho sio malengo].Ni muhimu kukumbuka kwamba malengo yetu hutegemea sana na utayari wetu wa kufanya kazi kwa ufanisi na kwa nguvu zote tulizonazo.

  • Fanya Jambo Moja Kwa Wakati Mmoja: Imeshawahi kukutokea jua linazama na upo njiani kuelekea nyumbani na unahisi umechoka kupita kiasi na huwezi kukumbuka kitu ulichofanikiwa kukifanya na kukimaliza katika siku inayorejea kwa Muumba? Jibu lako laweza kuwa ndio. Kinachotokea katika mazingira ya namna hiyo ni kwamba ulijaribu kufanya kila kitu kwa wakati mmoja.Pamoja na ukweli kwamba sote tungependa sana kutimiza mambo mengi kwa wakati mmoja [na wengi huwa tunasema we are multi-taskers], ukweli hatari zaidi ni kwamba akili zetu hazijaumbwa hivyo. Unapoanza kufanya jambo moja na ghafla ukashika lingine,akili yako nayo hugeukia upande huo.
Uwezo wetu unakuwa maradufu tunapofanya kitu kimoja kwa wakati mmoja badala ya kujaribu kurukia mambo kumi kwa wakati mmoja. Tunao msemo usemao “mtaka yote hukosa yote”. Ni kweli kabisa. Malengo tunayojiwekea ni ya aina nyingi. Kuna ya muda mfupi na muda mrefu. Yote yanahitaji kutulia kwa akili zetu. Jitahidi kukamilisha jambo moja kabla ya kurukia lingine. Utagundua kwamba kwa kufanya hivyo unakamilisha mambo mengi zaidi. Unashauriwa kugawa siku yako katika vipindi vya muda. Jiambie kwamba katika saa hii nitakachofanya ni kujibu barua pepe zangu. Katika saa inayofuatia, nitakuwa kwenye mkutano. Utatimiza mengi zaidi. Mbinu nzuri pia ni kuziweka katika muda fulani kazi au majukumu yanayoshabihiana. Kwa mfano kama unafanya kazi za ubunifu, weka mambo yanayoendana na ubunifu kwa wakati mmoja tofauti na masuala ya utawala, kwa mfano.

  • Maliza Jukumu, Achana Nalo, Gawa Majukumu, Aihirisha: Kimsingi kuna njia nne za kukamilisha jambo au jukumu. Aidha unalimaliza, unaachana nalo,unampa mtu mwingine au unalipa wakati tofauti au kwa kifupi unaliahirisha. Unapojiwekea malengo, ni muhimu pia kuangalia uwezo wako katika kukamilisha malengo hayo. Endapo wewe tu ndio mwenye uwezo na rasilimali za kukamilisha lengo au malengo fulani,basi fanya hivyo. Lakini endapo unahisi, kwa sababu moja au nyingine ikiwemo uwezo na rasilimali, huwezi kukamilisha jambo,basi usisite kugawa jukumu hilo kwa mtu mwingine.

Kugawa jukumu kwa mtu mwingine ni njia nzuri na mbadala ya kukamilisha lengo. Lakini pia usisite kuahirisha kufanya jambo fulani katika wakati fulani hususani kama halina umuhimu zaidi ya lingine. Na usijisikie vibaya.Hujashindwa. Umelisogeza mbele au kulipa wakati mwingine. Na mwisho kama unahisi lengo fulani halina umuhimu tena, basi achana nalo.

  • Badilisha Tabia na Mienendo: Tabia au mienendo yaweza kuwa kitu ambacho unataka kuacha kufanya, au unataka kuanza kufanya au unavyotaka kufanya zaidi au kwa uchache zaidi. Tukubali au tukatae,baadhi ya tabia au mienendo ni sumu katika mafanikio au malengo tunayojiwekea. Na kwa bahati mbaya zaidi,tabia hujijenga kwa muda na hivyo ni ngumu pia kuachika.

Je,ni tabia au mienendo gani ambayo unahisi inahatarisha malengo yako? Jibu, bila shaka, unalo wewe mwenyewe. Ninachoweza kukwambia ni kwamba anza sasa na haraka kukabiliana na tabia hiyo au hizo. Unashauriwa kuifanyia kazi moja baada ya nyingine [kama unazo zaidi ya moja]. Njia nzuri ni kuangalia vitu vinakusababishia tabia au mwenendo huo. Unapojiwekea malengo ya kupunguza uzito, kwa mfano, njia nzuri ni kufanya mazoezi, kuangalia mlo wako na kupumzika kwa wakati. Je, ni vitu gani vinakufanya malengo hayo yakwame? Anza kwa kuchunguza vyanzo hivyo na vifanyie kazi au epukana navyo kimoja baada ya kingine.


  • Ipe Akili Yako Taswira Ya Kufanikisha Lengo Au Malengo Yako: Imeshawahi kukutokea ukatamani au kuwa katika harakati ya kununua kitu [mfano gari] kisha baada ya muda mfupi tu ukawa unaliona hilo gari kila sehemu unayopita? Kinachotokea ni kwamba unakuwa umeipa akili yako taswira ya kile kitu. Hali ni hiyo hiyo katika malengo.

Unapotaka kufanikisha kitu fulani, huna budi kuipa akili yako taswira ya matokeo. Jione ulivyo na furaha zaidi pindi utakapokamilisha ndoto au lengo lako. Iambie au ielekeze akili yako[jielekeze] kule unapotaka kufika. Iambie akili yako kitu unachotaka. Kwa ujumla wake, unaweza kuhusisha hili na suala zima la kujiwekea malengo. Bila malengo na mipango ya kutimiza hayo malengo,bila shaka mengi yangekwama.

  • Fanya Uamuzi wa Kutimiza Lengo: Sababu mojawapo ya kushindwa kutimiza malengo yetu ni kutofanya uamuzi wa dhati wa kuanza kuyafanyia kazi malengo yetu. Mara nyingi utakuta,baada ya kuwa tumeshapanga mipango madhubuti kabisa, sehemu fulani ya akili zetu inaanza kutuambia “hatuwezi”. Kwamba hatuna ujuzi au uwezo wa kutosha. Tusubiri mpaka mwakani. Au tukusanye kwanza nguvu na rasilimali au taarifa za kutosha zaidi.

Generali mstaafu wa Marekani, Collin Powell, aliwahi kuulizwa kuhusu suala hili la maamuzi na akasema “Usisubiri mpaka utakapokuwa na taarifa,rasilimali nk kwa asilia mia moja kwani ukifanya hivyo unaweza kukuta umechelewa kabisa, badala yake ukishakuwa na asilimia arobaini tu ya taarifa,maarifa au chochote unachohitaji, anza.Mengine nenda kulingana na mazingira na akili yako inavyokutuma”

Unapojiambia kwamba nitakwenda kufanya jambo A au B, tayari unakuwa umejipa nguvu za ziada. Uamuzi ni muhimu.Amua kufanya jambo fulani kisha nenda kalifanye.

  • Jiulize Kwanini Unataka Kutimiza Malengo Unayojiwekea: Unataka kuwa bilionea? Kwanini? Mara nyingi huwa tunajiwekea malengo bila kujiuliza kwa makini sababu zinazotufanya tujiwekee malengo hayo. Matokeo yake, tunapoteza motisha mapema. Hatukujiuliza kwa makini kwanini au tulipojijibu hatukupata majibu kamili na yanayojitosheleza. Pengine yalikuwa ni matamanio tu na sio malengo halisi.

  • Chukua Hatua: Vitendo huongea zaidi ya maneno. Sasa ni wakati wa kuchukua hatua stahili. Malengo ni kama vile mradi. Lazima uwe umeandikwa vyema na uwe na vitu kama tarehe za kukamilisha na kila aina ya watu ambao wapo tayari kushirikiana nawe au unaopanga kuwashirikisha katika kutimiza lengo. Katika mradi[lengo] lako, ni hatua gani inapaswa kuanza? Chukua hatua hiyo. Jenga msingi huo. Ianze safari

  • Hujui Kila Kitu, Jifunze: Wakati mwingine ni vigumu kutambua kwamba, kama binadamu, tuna mapungufu chungu mbovu. Mara nyingi huwa ipo tamaa ya kuweza kufanya kila kitu. Tamaa ya aina hiyo ni sumu na ni chanzo cha kushindwa. Kuwa tayari kusikiliza na kujifunza kutoka kwa wengine. Kuwa tayari kujifunza kwa kushirikiana na wengine au kugawa majukumu. Amini wengine na amini kwamba pamoja na jitihada zako zote, yaweza kuwepo mtu au watu wengine ambao wanajua zaidi.

  • Nidhamu: Yote tisa,kumi ni nidhamu. Malengo yoyote tunayojiwekea ni rahisi kuyatimiza endapo tu tutakuwa na nidhamu ya kufuata na kufanya yale yote tunayotakiwa kuyafanya. Nidhamu ni uwanja mpana. Kuna wakati tunakuwa hatuna nidhamu.Bahati nzuri ni kwamba kwenye suala la nidhamu tunaweza kujifunza. Kama nilivyogusia kwenye tabia[ ambazo nyingine hupekelea au hutokana na ukosefu wa nidhamu]

Kuna mbinu zaidi ya 10. Unaweza kujifunza zaidi. Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kutimiza malengo na kufanikiwa.

No comments:

Post a Comment